Wakaazi wa Kisumu Ndogo mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, wamelalamikia ongezeko la taka zinazotupwa karibu na shule mbili za msingi, wakisema hali hiyo inahatarisha afya ya wanafunzi na kutatiza shughuli za masomo pamoja na usafiri katika barabara ya Airport–Furunzi.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi, balozi wa Nyumba Kumi Jacinta Nduta alisema taka hizo zinaendelea kuongezeka na huenda zikachochea mlipuko wa magonjwa. Pia alieleza wasiwasi kuhusu msitu uliopo karibu na eneo hilo ambao unadaiwa kuhusishwa na visa vya uhalifu.

AdvertisementIn-article placement — advertise with Kilele Radio

Mkaazi mwingine, Kelvin Lenku, alitaka usafi kudumishwa na taa za barabarani kuwekwa ili kuboresha usalama na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Wakazi hao wameitaka serikali ya kaunti na idara ya manispaa kuchukua hatua za haraka kutatua tatizo hilo ambalo wanasema limekuwa kero kwa muda mrefu.