
Vijana wametakiwa kuepuka uvunjaji wa sheria na vitendo vya uhalifu wakati wa maandamano yatakayofanyika kesho ya kuwakumbuka vijana wa Gen-Z waliofariki katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024/2025.
Akizungumza katika mkutano wa vijana ulioandaliwa na Siasa Space kwa ushirikiano na Agenda Kenya, mwaniaji wa ubunge wa Changamwe, Hassan Mbangwe Athman, amesema kuwa ingawa Katiba ya Kenya inaruhusu maandamano ya amani, ni muhimu kwa vijana kudumisha nidhamu, kuwajibika na kuheshimu sheria.
Athman pia amewataka viongozi wa kisiasa kuepuka kuwachochea vijana kushiriki katika vitendo vya vurugu, na badala yake kuhamasisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa. Aidha, ameyapongeza mashirika hayo kwa kuandaa mafunzo yanayowasaidia vijana kujiandaa kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, afisa wa Siasa Space, Monica Atieno, amewahimiza wanawake na vijana kuwa makini na kujilinda dhidi ya vitisho vya kimtandao wanaposhiriki katika shughuli za siasa na uongozi.
Vijana walioshiriki mafunzo hayo wamesema kuwa yamewaongezea maarifa, ujasiri na kujiamini katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za mitandaoni, hususan zile zinazohusiana na usalama wa kidijitali.