By:Hassan Pojjo

Abukar Mohamed Abdullahi amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Dock Workers Union baada ya kushinda uchaguzi wa viongozi wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni.
Abdullahi alipata kura 1,042, na kumshinda mpinzani wake pekee, Salim Kumaka, aliyepata kura 581. Atahudumu kwa kipindi cha miaka mitano akiongoza masuala ya wafanyakazi wa bandarini na kusimamia utekelezaji wa ajenda za chama.

Katika nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, Gunda Kaneno alishinda kwa kura 825, dhidi ya Hassan Shabura aliyepata kura 774.
Abdalla Randani alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa baada ya kupata kura 597, akifuatiwa na Moris Mayega mwenye kura 409, Shafi Ali kura 404 na Amini Muasya kura 179.
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Msaidizi ilichukuliwa na Gideon Matiku, aliyepata kura 1,079, dhidi ya Rashid Mwagasare aliyepata kura 497.
Matokeo hayo yalitangazwa na Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Dock Workers Union, Renson Toya, baada ya kura kutoka vituo mbalimbali katika maeneo yanayohudumiwa na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) kujumlishwa.

Abdullahi: Hatukuja Kupigana na KPA
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa ushindi wake, Abdullahi alisema uongozi mpya hautaingia madarakani kwa lengo la kuanzisha migogoro na menejimenti ya KPA, bali utalenga kujenga mazungumzo, ushirikiano na suluhu kwa changamoto zinazowakabili wafanyakazi.
Alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Captain William Ruto, kwa kile alichosema ni kujitolea katika kushughulikia masuala yanayowahusu wafanyakazi na chama hicho.
Abdullahi alisema ushindi huo unaashiria mwanzo wa ukurasa mpya katika Dock Workers Union, akiahidi kurejesha imani ya wanachama na kuweka ustawi wao mbele.
“Hatukuja kupigana na KPA.”
Alisema lengo ni kujenga “Dock Workers Union ya kizazi kipya” yenye uwezo wa kuwakilisha wafanyakazi na kushughulikia changamoto zao kwa ufanisi.
Kaneno Aonya Dhidi ya Migogoro
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Taifa, Gunda Kaneno, alisema uongozi wake utalenga kupunguza migogoro isiyo ya lazima kati ya chama cha wafanyakazi na menejimenti ya KPA.

Kaneno alisema migogoro ya mara kwa mara inaweza kuathiri shughuli za Bandari ya Mombasa, ambayo ni lango muhimu la biashara kwa Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Kati.
Alisisitiza umuhimu wa mazungumzo na ushirikiano katika kushughulikia masuala ya ajira, ustawi na mazingira ya kazi.
Viongozi Wengine Wachaguliwa
Katika uchaguzi huo, Said Mitsumi, Monica Wanjiru na Austin Ogolla walichaguliwa kushika nafasi za Executive Zone 6, Gender Zone 7 na Executive Zone 8 mtawalia.
Viongozi 17 walichaguliwa bila kupingwa katika nafasi mbalimbali, wakiwemo Idd Yusuf Mchangamwe kama Treasurer, Naheel Hashil kama Assistant Treasurer, Nuru Awadh kama Gender Chairperson, Ramadhan Tadicha kama Male Young Worker na Joan Kiprop kama Female Young Worker.

Uongozi mpya sasa una jukumu la kuunganisha wanachama, kuimarisha uwakilishi wa wafanyakazi, kuboresha ustawi wao na kujenga mahusiano yenye tija na menejimenti ya KPA.
Viongozi hao watakuwa madarakani kwa miaka mitano, huku wanachama wakitarajia utekelezaji wa ahadi za kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa bandarini.