By:Hassan Pojjo

Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Makande imepokea vifaa mbalimbali vya masomo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Maeneo Bunge wa NG-CDF Mvita, katika juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwapa wanafunzi ujuzi wa kisasa.

Vifaa vilivyokabidhiwa na Mbunge wa Mvita, Mohammed Masoud Machele, ni pamoja na kompyuta 20, viti 21 vya ukumbi, mashine 20 za kushonea pamoja na runinga janja ya inchi 55.

Machele amesema msaada huo unalenga kuimarisha elimu ya kidijitali, kukuza ujuzi wa vitendo na kuwaandaa wanafunzi kwa fursa za baadaye.

Amesisitiza kuwa elimu itaendelea kuwa kipaumbele katika maendeleo ya eneo la Mvita kupitia miradi inayotekelezwa na NG-CDF.

Katika hafla hiyo, mbunge huyo aliambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya NG-CDF Mvita, Ali Bafundi, pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo.
