
By:Hassan Pojjo
Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, ameitaka serikali kuimarisha utekelezaji wa viwango vya upatikanaji wa huduma katika majengo ya umma na ya kibiashara nchini ili kuhakikisha watu wanaoishi na ulemavu hawabaguliwi katika kupata huduma.
Akizungumza bungeni, Badi alisema ameomba taarifa rasmi kuhusu kiwango cha utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohakikisha majengo yote yanakuwa na miundombinu rafiki kwa watu wote, ikiwemo njia maalum za walemavu, lifti, alama elekezi na huduma nyingine muhimu.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha majengo ya umma na yale ya kibinafsi yanazingatia viwango vya kitaifa vya upatikanaji wa huduma, ili kila Mkenya aweze kufikia huduma bila vikwazo.
Aidha, ametaka kubainishwa iwapo kuna ukaguzi wa mara kwa mara wa majengo nchini ili kuhakikisha yanazingatia sheria za ujenzi na upatikanaji wa huduma kwa wote, pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wamiliki wanaokiuka masharti hayo.
Badi amesema maendeleo ya miji na miundombinu yanapaswa kwenda sambamba na usawa, ujumuishi na kulinda haki za watu wote, hususan watu wanaoishi na ulemavu.
Ameeleza kuwa hatua madhubuti za utekelezaji wa sheria zitasaidia kuhakikisha majengo yote yanawafaa Wakenya wote bila ubaguzi.