By:Alii Vincent

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imerejesha mali za umma zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 baada ya kushinda kesi mbili za unyakuzi wa ardhi katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi za Mombasa na Kwale.
Akizungumza Diani, Kaunti ya Kwale, Katibu Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa EACC, Abdi Mohamud, alisema mali zilizorejeshwa ni nyumba ya serikali iliyoko Kizingo, Mombasa yenye thamani ya shilingi milioni 55, pamoja na eneo la njia ya umma inayoelekea ufukweni Diani, Kwale lenye thamani ya shilingi milioni 45.
Mohamud amesema mahakama hizo pia ziliwatia hatiani baadhi ya maafisa wa zamani wa Wizara ya Ardhi waliotumia vibaya mamlaka yao kuwezesha ugavi usio halali wa mali hizo.
Kwa mujibu wa EACC, uchunguzi ulibaini kuwa nyumba ya serikali ya Kizingo iligawiwa kwa njia ya udanganyifu mwaka 1998, huku eneo la njia ya umma kuelekea ufukweni Diani likitwaliwa isivyo halali na kampuni binafsi mwaka 1994.
Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani amesema serikali za kaunti zina wajibu wa kushirikiana na EACC ili kulinda mali za umma dhidi ya unyakuzi na matumizi mabaya.
Mohamud amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, EACC imefanikiwa kurejesha mali za umma zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.16 katika ukanda wa Pwani. Ameongeza kuwa tume itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi na unyakuzi wa mali za umma ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa kwa manufaa ya Wakenya wote.