By:Alii Vincent

Takriban mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, kuzindua ujenzi wa shule ya awali katika eneo la Maganda, Jomvu, Kaunti ya Mombasa, mkewe Ida Odinga amefungua rasmi jengo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Ida Odinga amewapongeza viongozi wa Kaunti ya Mombasa wakiongozwa na Abdulswamad Shariff Nassir pamoja na Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, kwa kuweka elimu miongoni mwa vipaumbele vya maendeleo. Pia amewahimiza wazazi kuwasajili watoto wao katika shule hiyo ili wanufaike na elimu bora ya awali.

Kwa upande wake, Mbunge Badi Twalib amesema mradi huo unaakisi dhamira ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa ya kuendelea kuwekeza katika elimu ya awali ili kuwajengea watoto msingi imara wa maendeleo yao ya baadaye.

Mbunge huyo ameongeza kuwa inatia moyo kuona maono yaliyoanzishwa kwa kuwekwa kwa jiwe la msingi na Raila Odinga sasa yametimia na kuwa manufaa kwa wakazi wa Maganda na maeneo jirani. Ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo kuimarisha sekta ya elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto.

Naye Gavana Abdulswamad Shariff Nassir amesema serikali ya kaunti itaendelea kuwekeza katika elimu kupitia utoaji wa elimu ya bure ya awali, chakula shuleni na vitabu, ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
