By:Glory Mwagambo

Wakazi wa eneo la Furunzi, mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi, wamelalamikia kile wanachodai kuwa ni uzembe wa serikali katika kushughulikia changamoto zinazosababishwa na Ziwa la Furunzi, ambalo wanasema limekuwa likihatarisha afya na maisha yao kwa muda mrefu.

AdvertisementIn-article placement — advertise with Kilele Radio

Akizungumza kwa niaba ya wakazi, Walter Kyalo alisema kuwa licha ya ziwa hilo kuwa na manufaa mbalimbali kwa jamii, serikali inapaswa kuchukua hatua za kulihifadhi na kulitumia ipasavyo. Alisema maji ya ziwa hilo yanaweza kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa maji linaloikumba eneo hilo iwapo yatahifadhiwa kupitia ujenzi wa mabwawa na miundombinu mingine.

Hata hivyo, wakazi hao wanasema wakati wa mvua nyingi ziwa hilo hufurika na kusababisha kuzuka kwa magonjwa pamoja na kuhatarisha usalama wa jamii. Wameeleza masikitiko yao kwa kile wanachokitaja kuwa ni ukosefu wa mwitikio kutoka kwa viongozi wao wa kisiasa, hususan wabunge, kila wanapohitaji msaada.

Wakazi hao wamewashutumu viongozi wao kwa kuwapuuza kwa muda mrefu, wakisisitiza kuwa wao pia ni wananchi na wapiga kura wenye haki ya kupata huduma na maendeleo kama maeneo mengine.

Kwa upande wake, Evans Gili, ambaye pia ni mkazi wa Furunzi, amewataka wazazi kuwa waangalifu zaidi kwa watoto wao wanaocheza kandokando ya ziwa hilo, hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi, ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea.

Aidha, Gili amesema kuwa pamoja na changamoto zilizopo, Ziwa la Furunzi linaweza kuwa rasilimali muhimu ikiwa serikali itajenga mabwawa na kuweka mikakati ya kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadaye.

Wakazi hao wameendelea kutoa wito kwa serikali pamoja na mashirika mbalimbali kuingilia kati haraka na kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazotokana na ziwa hilo, wakisema kuwa wamekuwa wakisubiri msaada huo kwa muda mrefu bila mafanikio.