
Mwaniaji wa kiti cha uwakilishi wa wanawake Mombasa, Amina Abdalla, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya maeneo yao ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakidhi mahitaji yao halisi.
Akizungumza katika baraza la umma kuhusu Mpango wa Makazi wa Kibarani, Amina alisema kuwa maoni ya wananchi yana mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo endelevu na kuimarisha ustawi wa jamii.
Ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya wakazi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Baraza hilo pia liliwapa wakazi fursa ya kueleza maoni yao na kuwasilisha changamoto wanazokumbana nazo, huku viongozi wakiahidi kushughulikia masuala yaliyoibuliwa kwa njia inayozingatia maslahi ya wananchi wote.
Katika mkutano huo, Amina Abdalla aliungana na Badi Twalib, Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Jomvu, Kamishna Msaidizi wa Kaunti pamoja na viongozi wa eneo na wakazi wa Kibarani kujadili masuala yanayohusu Mpango wa Makazi wa Kibarani.