By:Hassan Pojjo

Wananchi wa Wadi ya Kipevu watanufaika na huduma bora, fursa zaidi za kiuchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo endapo viongozi wataweka mbele maslahi ya wananchi badala ya siasa, amesema kiongozi wa Wiper na mwaniaji wa nafasi ya Uwakilishi wa Wadi hiyo, Faith Mwende Boniface.
Akizungumza baada ya kukutana na wakazi wa eneo hilo, Faith alisema kipaumbele chake ni kuboresha maisha ya wananchi kupitia uongozi unaozingatia uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi na utoaji wa huduma bora.
Alisema ataendelea kutetea miradi ya kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalumu kiuchumi, pamoja na kushinikiza kuboreshwa kwa huduma za elimu, afya, mazingira safi na uundaji wa nafasi za ajira.

“Kiongozi wa kweli ni yule anayebadilisha maisha ya wananchi kupitia matendo na si ahadi pekee. Imani waliyonionyesha wananchi inanipa nguvu ya kuendelea kuwatumikia,” alisema.
Faith alibainisha kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila ushirikiano kati ya viongozi na wananchi, akiwataka wakazi kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya eneo lao.
Aliwashukuru wananchi kwa mapokezi na uungwaji mkono waliompa, akisema ni ishara ya imani waliyonayo katika ajenda yake ya maendeleo.
Aliahidi kuendelea kuwa sauti ya wakazi wa Wadi ya Kipevu na kusukuma sera na miradi itakayoboresha maisha yao endapo atachaguliwa.