By:Hassan Pojjo

Huku suala la ardhi likiwa donda sugu katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani wakaazi wa eneo bunge la Jomvu wanaendelea kupewa hamasa na viongozi wao.
Katika juhudu za kuimarisha na kutatua changamoto za ardhi katika eneo bunge mbunge wa eneo hilo Badi Twalib, amefanya baraza la wananchi na wakazi wa eneo la KCC, Wadi ya Miritini, kujadili masuala ya umiliki wa ardhi pamoja na utekelezaji wa agizo la Rais William Ruto la siku 90 la kuharakisha mchakato wa uhakiki na umilikishaji wa ardhi katika Ukanda wa Pwani.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa eneo hilo pamoja na mamia ya wakazi, Mbunge huyo aliwahakikishia wananchi kuwa zoezi la uhakiki wa umiliki wa ardhi litapanuliwa na kuwafikia wakazi wa KCC na Miritini ili kuhakikisha hakuna mwananchi atakayebaguliwa katika mchakato huo muhimu.
Badi alisema Serikali imejizatiti kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi kwa miaka mingi.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa agizo la Rais unalenga kuhakikisha wananchi wanapata hati miliki halali na kuondoa migogoro inayochelewesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, aliwataka wananchi wote wenye kesi za ardhi mahakamani kutafuta njia za maelewano na kusuluhisha tofauti zao kwa amani ili kuruhusu shughuli za upimaji wa ardhi na uhakiki kuendelea bila vikwazo.
Alieleza kuwa ushirikiano wa wananchi utaharakisha mchakato huo na kuhakikisha wakazi wa KCC wananufaika kikamilifu na mpango huo wa serikali.
Mbunge huyo alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais William Ruto ya kumaliza changamoto za ardhi katika eneo la Pwani, ambapo serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha wananchi wanapata haki ya kumiliki ardhi wanayoishi na kuendeleza maisha yao kwa utulivu.

Kwa upande wao, wakazi waliohudhuria mkutano huo walieleza matumaini yao kuwa zoezi hilo litamaliza migogoro ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakosesha fursa ya kuendeleza ardhi zao na kupata hati miliki.
Pia waliomba viongozi na maafisa wa serikali kuhakikisha mchakato unafanyika kwa uwazi, haki na ushirikishwaji wa wananchi wote.
Baraza hilo pia lilihudhuriwa na Diwani wa Wadi ya Miritini, Mheshimiwa Kibwana Swaleh Baya, pamoja na viongozi wa Utawala wa Kitaifa (NGAO) wakiongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo wa Miritini (ACC), Bw. Sayanka. Viongozi wengine waliokuwepo ni Chifu Rama, Chifu Bi. Asha pamoja na wazee wa kijamii na wakazi wa eneo hilo.
Mkutano huo ulimalizika kwa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha zoezi la uhakiki, upimaji na umilikishaji wa ardhi linafanikiwa na kuleta suluhisho la kudumu kwa changamoto za ardhi zinazowakabili wakazi wa KCC na maeneo jirani.