By:Glory Mwagambo

Viongozi wa dini ya Kiislamu mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, wamepinga vikali kufanyika kwa tamasha la Summertide linalotarajiwa kufanyika Jumamosi hii kwa awamu ya pili, wakidai kuwa linaweza kuathiri maadili ya jamii na mwelekeo wa vijana.
Wakizungumza mjini Malindi, viongozi hao wakiongozwa na Famau Mohamed, kiongozi wa dini ya Kiislamu na mwanaharakati wa kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, wamesema serikali haipaswi kuangalia matukio kama hayo kwa upande wa mapato ya utalii pekee, bali pia kuzingatia athari zake kijamii.
Famau amesema kuwa kuna haja ya kufanyika tathmini ya kina kabla ya kuruhusu matukio yanayoweza kuibua mjadala kuhusu maadili ya jamii, akisisitiza kuwa kuna njia nyingine za kukuza uchumi bila kuathiri misingi ya tamaduni za jamii.
Hata hivyo, viongozi hao wamesema hawapingi utalii wala ujio wa wageni katika eneo la Pwani, bali wanapinga baadhi ya mienendo wanayodai kuambatana na tamasha hilo, ikiwemo mavazi na tabia wanazosema haziendani na mila, desturi na maadili ya jamii ya Pwani.
Kwa upande wake, msomi wa dini ya Kiislamu na mchambuzi wa masuala ya siasa, Shaban Maalim, ameitaka serikali kuweka mbele ustawi wa jamii wakati wa kutoa vibali kwa matukio ya burudani, akisema maamuzi hayo yanapaswa kuzingatia athari zake kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Viongozi hao wameitaka serikali kufanya tathmini ya kina kuhusu tamasha hilo na kuhakikisha kuwa maslahi mapana ya jamii, utamaduni na maadili yanazingatiwa katika maamuzi yake.