By:Hassan Pojjo

Waumini na wadau wa Kanisa Katoliki la St. Joseph Tudor, Mombasa, wamejitokeza kuchangia fedha katika hafla maalum ya kuunga mkono utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa kanisa hilo.
Hafla hiyo ya chakula cha kuchangisha fedha ilifanyika katika Pastoral Center Hall, Tudor, na kuhudhuriwa na viongozi wa kanisa, waumini, marafiki pamoja na wadau mbalimbali wenye nia ya kusaidia maendeleo ya taasisi hiyo ya kidini.
Mgeni wa hafla hiyo, Mbunge wa Mvita Mohammed Masoud Machele, alitoa mchango wake huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano katika kufanikisha miradi ya maendeleo.

Machele alisema taasisi za kidini zina nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na uwajibikaji, mbali na kutoa huduma zinazowanufaisha wananchi.
Alisema ushirikiano kati ya viongozi, taasisi za kidini, waumini na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa mafanikio na kuwa na manufaa ya muda mrefu.
Mbunge huyo aliipongeza uongozi wa Kanisa la St. Joseph Tudor pamoja na waumini kwa kuandaa hafla hiyo, akisema kila mchango una umuhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo yaliyowekwa.

Aidha, aliwahimiza wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono taasisi za kidini katika miradi inayolenga kuboresha huduma na ustawi wa jamii.
Hafla hiyo pia ilitumika kuimarisha mshikamano miongoni mwa waumini na wadau wa kanisa, huku washiriki wakitoa michango yao kwa ajili ya kuhakikisha mpango wa maendeleo wa St. Joseph Tudor unatekelezwa.

Machele alisema miradi hiyo itakuwa na manufaa si kwa waumini wa sasa pekee, bali pia kwa vizazi vijavyo, akisisitiza umuhimu wa kuweka misingi imara ya maendeleo endelevu.