By Hassan Pojo

Mashindano ya Digital Kickoff Tournament, yanayofadhiliwa na Mheshimiwa Dkt. Omondi Obuya, yanaendelea kushika kasi huku yakishuhudia matokeo ya kushtua ambapo baadhi ya timu kubwa zimeangushwa na timu ndogo.

AdvertisementIn-article placement — advertise with Kilele Radio

Akizungumza na Kilele Viwanjani, msimamizi wa mashindano hayo Joseph Oluoch amesema michuano hiyo imewaleta pamoja vijana na jamii huku ikitoa fursa ya kukuza vipaji.

Katika matokeo ya siku hiyo, Forever FC iliichapa Mikindani Legend bao 1-0, Young Rovers ikaifunga Mikindani FC mabao 2-1, Boda Boda FC na Mwembeni FC zikatoka sare ya 1-1, huku Staff Boyz ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mabati FC.

Mashindano hayo yanaendelea kuvutia mashabiki wengi na yanakusudia kukuza vipaji, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuwapa vijana jukwaa la kuonyesha uwezo wao.

Katika mchezo wa gofu, Mnyarwanda Jean D’Amour Hitayezu ametwaa ubingwa wa mashindano ya NCBA Coast Open ‘Barry Cup’ yaliyofanyika Nyali Golf and Country Club, Mombasa, baada ya kumaliza mbele ya John Kamaisi wa Nakuru Golf Club.

Licha ya kumaliza wa pili, Kamaisi ameendelea kuongoza msimamo wa Kenya Amateur Golf Championship Order of Merit akiwa na alama 809.20. Mashindano hayo yaliwakutanisha wachezaji bora kutoka Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki na kuongeza ushindani kuelekea michuano ijayo.

Katika kriketi, Washington Freedom imehitimisha hatua ya makundi ya Major League Cricket nchini Marekani kwa ushindi wa wiketi tano dhidi ya MI New York.

Washington Freedom ilifikia lengo la mikimbio 188 katika over 18.3 baada ya MI New York kuweka mikimbio 187 kwa kupoteza wiketi nane. Andries Gous aling’ara kwa mikimbio 96 bila kutolewa, akisaidiwa na Rachin Ravindra aliyefunga 60, huku Nicholas Pooran akiongoza MI New York kwa mikimbio 86. Ushindi huo umeihakikishia Washington Freedom nafasi ya kutinga hatua ya mtoano.