By:Hassan Pojjo

Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) Tawi la Mombasa, Alamin Ahmed Abdallah, ameendeleza juhudi za kutambua, kukuza na kuibua vipaji vya soka miongoni mwa vijana wadogo katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Mombasa.
Alamin amekuwa akifanya ziara katika maeneo tofauti ya kaunti kwa lengo la kukutana na wachezaji chipukizi, kuwapa hamasa pamoja na kuwaelekeza kuhusu umuhimu wa kutumia vipaji vyao kwa njia yenye manufaa kwa maisha yao ya baadaye.
Katika ziara yake iliyoanzia eneo la Mtongwe, Likoni, Alamin alikutana na wachezaji wenye umri wa miaka 13, ambapo alifanya nao mazungumzo yenye lengo la kuwajenga kisoka na kimaisha.

Akizungumza na vijana hao, Alamin aliwasisitiza umuhimu wa kutumia kila fursa inayojitokeza katika maisha yao ili kuonyesha uwezo wao na kupiga hatua kutoka ngazi ya mashinani hadi kwenye viwango vya juu vya soka.
“Ni muhimu nyinyi kama vijana mkipata fursa ya kuonyesha talanta zenu ili muweze kuinuka katika ngazi za juu. Vilevile msisahau kutia bidii katika masomo, kwani ndio yatakayowapa ngazi ya kufikia ndoto zenu katika mpira,” alisema Alamin.
Alamin pia aliwataka vijana kuwa na nidhamu na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na safari yao ya kimichezo.

Aliwahimiza kutumia muda wao katika michezo na shughuli nyingine chanya badala ya kujiingiza katika matumizi ya mihadarati na vitendo vya kihuni.
“Tujitahidi tuache mihadarati na uhuni na tucheze mpira. Kwa neno moja, Wacha Panga, Vaa Njumu,” alisisitiza.
Ampongeza Hamza Lali Katika ziara hiyo, Alamin pia alimtaja na kumpongeza kijana Hamza Lali, mwenye umri wa miaka 16, ambaye licha ya kuwa mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Likoni, amekuwa akijitolea katika urefa wa michezo pamoja na kucheza soka.

Hamza anatajwa kuwa na ndoto ya kuendelea na shughuli za urefa na soka katika siku zijazo, jambo ambalo limevutia umakini wa uongozi wa FKF Mombasa.
Alamin ameahidi kumsaidia Hamza kupata mafunzo ya urefa ili aweze kuongeza ujuzi na maarifa katika eneo hilo.
Aidha, amesema juhudi hizo hazitalenga Hamza pekee, bali pia wakufunzi chipukizi wanaohitaji kupata elimu na mafunzo yatakayowawezesha kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Kwa mujibu wa Alamin, uwekezaji katika vijana haupaswi kuishia kwa wachezaji pekee, bali unapaswa kuwahusisha pia marefa, makocha na wadau wengine wanaosaidia kuendeleza soka kutoka ngazi ya mashinani.
Baada ya Mtongwe, ziara ya Alamin iliendelea katika Uwanja wa Mbuzi, mtaa wa Nyali, ambako aliendelea kukutana na vijana na wadau wa soka katika eneo hilo.
Ziara hizo zinaangazia umuhimu wa kuimarisha soka la vijana kutoka ngazi za chini, huku vijana wakipewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao, kupata ushauri na kuelekezwa namna ya kutumia vipaji hivyo kujenga maisha yao ya baadaye.
Alamin amesema juhudi za FKF Mombasa zitaendelea kulenga maeneo mbalimbali ya kaunti ili kuhakikisha vipaji vilivyoko mashinani vinatambuliwa na kupewa nafasi ya kukua.

Hatua hiyo inalenga kuibua kizazi kipya cha wachezaji, marefa na makocha ambao wanaweza kuiwakilisha Mombasa katika mashindano ya ngazi ya kaunti, kitaifa na hata kimataifa.
Kwa vijana wa Mombasa, ziara hizo zinaendelea kutoa ujumbe kwamba vipaji vyao vinaweza kuwa na nafasi katika soka endapo watakuwa na nidhamu, bidii, elimu na utayari wa kutumia fursa zinazojitokeza.