By:Athuman Luchi

Madereva wa teksi za kidijitali mjini Mombasa wameipa kampuni ya Bolt siku tatu kurekebisha nauli zilizopunguzwa, wakitishia kusitisha huduma ikiwa madai yao hayatashughulikiwa.

AdvertisementIn-article placement — advertise with Kilele Radio
Voiced Package

Madereva hao wanapinga pia kuanzishwa kwa daraja la Basic, wakisema nauli ya chini ya shilingi 220 kwa safari haiendani na gharama za uendeshaji.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Coast Digital Drivers Federation, Thomas Were, wamesema kupanda kwa bei ya mafuta, gharama za matengenezo ya magari na hali ngumu ya maisha kumewaathiri.

Wanataka Bolt kuondoa daraja la Basic Pwani, kuweka nauli ya chini inayofaa, na kuhakikisha madereva wanalipwa kwa muda wa kusubiri abiria pamoja na safari zinazoghairiwa.

Aidha, wanataka kushirikishwa kabla ya kampuni hiyo kuanzisha sera mpya, pamoja na kuwepo kwa mfumo wa uwazi wa kusimamisha akaunti za madereva na kukata rufaa.

Madereva hao wamesema baadhi yao wamechukua mikopo ya kati ya shilingi milioni moja na mbili kununua magari na wanategemea biashara hiyo kugharamia familia zao.

Wameonya kuwa iwapo Bolt haitashughulikia malalamiko yao ndani ya siku tatu, watahamasisha kusitishwa kwa huduma za Bolt Mombasa.